Dua ya kuamka kutoka usingizini

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu ambae ametupa uhai baada ya kutufisha na nin kwake tu kufufuliwa. (Bukhar, katika Fathul-baar 11/113)

Hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu peke yake hana mshirika, ni wake Ufalme, na ni zake sifa njema, na Yeye juu ya kila kitu ni muweza, ametakasika Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni mkubwa na hapana uwezo wala nguvu isipokuwa vyote vinatokana na Mwenyezi Mungu aliye juu, aliye mtukufu, ewe Mola (Mwenyezi Mungu) nisamehe. ........Mwenye kusema hayo (wakati akishutuka kutoka usingizini) basi atasamehewa. Na kama atasimama akaenda kutawadha, akaswali basi swala yake itakubaliwa. (Bukhar, katika Fathul-baar 3/39 namba 1154, na wengineo. Na lafdhi ya Ibni Maajah, angalia: sahihi Ibni Maajah, 335/2.)

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu ambae amenipa uzima wa mwili wangu, na akanirudishia roho yangu, na akaniruhusu kumtaja. (Tirmidhy, 5/473, namba 3401, na angalia: sahihi Tirmidhy, 144/3.)

Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara kwa wenye akili* Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima na wakikaa kitako na wakilala, na hufikiri kuumbwa mbingu na ardhi, wakisema: Mola wetu Mlezi! Hukuviumba hivi bure. Subhanaka, Umetakasika! Basi tukinge na adhabu ya Moto* Mola wetu Mlezi! Hakika unaye mtia Motoni umemhizi; na walio dhulumu hawana wasaidizi* Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tumemsikia mwenye kuita akiitia Imani kwamba: Muaminini Mola wenu Mlezi; nasi tukaamini. Basi tusamehe madhambi yetu, na utufutie makosa yetu, na utufishe pamoja na watu wema* Mola wetu Mlezi! Na utupe uliyo tuahidi kwa Mitume wako, wala usituhizi Siku ya Kiyama. Hakika Wewe huvunji miadi* Mola Mlezi wao, akayakubali maombi yao akajibu: Hakika sipotezi kazi ya mfanya kazi miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke, kwani ni nyinyi kwa nyinyi. Basi walio hama, na walio tolewa makwao, na wakateswa katika Njia yangu, na wakapigana, na wakauliwa, kwa yakini Mimi nitawafutia makosa yao, na kwa yakini nitawaingiza katika Mabustani yanayo pita mito kati yake. Hayo ndiyo malipo yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu kwake yapo malipo mema kabisa* Kabisa kusikudanganye kubakia kutangatanga kwa walio kufuru katika nchi* Hiyo ni starehe ndogo. Kisha makaazi yao yatakuwa Jahannamu. Na ni mahali pabaya mno pa kupumzikia* Lakini walio mcha Mola wao Mlezi watapata Mabustani yanayo pita mito kati yake. Watadumu humo. Hayo ni makaribisho yao yatokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na vilioko kwa Mwenyezi Mungu ni bora kwa watu wema* Hakika miongoni mwa Watu wa Kitabu wapo wanao muamini Mwenyezi Mungu na yaliyo teremshwa kwenu na yaliyo teremshwa kwao, wakimnyenyekea Mwenyezi Mungu. Hawabadili Aya za Mwenyezi Mungu kwa thamani duni. Hao wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu*. Enyi mlio amini! Subirini, na shindaneni kusubiri, na kuweni macho, na mcheni Mwenyezi Mungu, ili mpate kufanikiwa. (Surat Al-Imran: 190-200)

API