Dua ya swalatul-Istikhara (swala ya kutaka maelekezo au kutaka ushauri katika jambo)

Amesema Jaabir bin Abdillah (r.a): Alikuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) akitufundisha swala ya Istikhara kama vile anavyotutufunza sura ya Qur'an, anasema (s.a.w): Akikusudia mmoja wenu kufanya jambo, aswali rakaa mbili zisizo za faradhi, kisha aseme: Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nakutaka muelekezo kwa ujuzi wako, na nakuomba uniwezeshe kwa uwezo wako, na nakuomba fadhila zako kubwa, hakika Wewe unaweza nami siwezi, nawe unajua nami sijui, na Wewe ni mjuzi wa yale yaliyo fichikana. Ewe Mwenyezi Mungu, iwapo jambo hili kutokana na ujuzi wako (atalitaja jambo lake) lina kheri na mimi katika dini yangu na maisha yangu na mwisho wa jambo langu (karibu au mbali) basi nakuomba uniwezeshe nilipate, na unifanyie wepesi, kisha unibariki, na iwapo unajua kwamba jambo hili ni shari kwangu katika dini yangu na maisha yangu na mwisho wa jambo langu (karibu au mbali) basi liepushe na mimi nami niepushe nalo, na nipangie jambo jengine lenye kheri na mimi popote lilipo kisha niridhishe kwalo. Na hajuti mwenye kumtaka muelekeo Mwenyezi Mungu, na akawashauri waja waumini, na akajidhatiti katika jambo lake. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kumwambia Mtume wake (s.a.w): {Na shauriana nao katika mambo. Na ukiazimia kufanya jambo basi mtegemee Mwenyezi Mungu} (Suratul-Imran: 159)

API