Fadhila za tasbiih, tahmiid, tahliil na takbiir

Amesema Mtume (s.a.w): ''Mwenye kusema: ''Ametakasika Mwenyezi Mungu na sifa njema zote ni zake.'' Kwa siku mara mia, atafutiwa madhambi yake hata kama yalikuwa mfano wa povu la bahari.

Na Mtume (s.a.w) amesema: ''Atakaesema:'' ''Hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu hali ya kuwa peke yake, hana mshirika, ni wake Ufalme, na ni zake kila sifa njema, na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza.'' ......Mara kumi, ni kama (thawabu za mtu) aliyeacha huru nafsi nne katika wana wa Ismail.

Na amesema Mtume (s.a.w): Kuna maneno mawili ni mepesi mno juu ya ulimi, mazito mno katika mizani, yanapendeza mno mbele ya Rahmani (Mwenye kurehemu) nayo ni: ''Ametakasika Mwenyezi Mungu, na sifa njema zote ni zake, ametakasika Mwenyezi Mungu aliye Mtukufu.''

Na amesema Mtume (s.a.w): ''Kusema kwangu: ''Ametakasika Mwenyezi Mungu, na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila ni Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mkubwa.'' .....Ni bora kwangu kuliko kila kilicho angaziwa na jua.

Na amesema Mtume (s.a.w): ''Hivi anashindwa mmoja wenu kuchuma kila siku thawabu elfu? Mtu mmoja miongoni mwa waliokaa akamuuliza: Atachuma vipi mmoja wetu thawabu elfu? (Mtume s.a.w) Akamjibu: Aseme: (Subhana LLah). ''Ametakasika Mwenyezi Mungu.'' ...Mara mia moja, basi ataandikiwa thawabu elfu moja, au atafutiwa madhambi elfu moja.

Na amesema Mtume (s.a.w): ''Atakaesema: ''Ametakasika Mwenyezi Mungu aliye Mtukufu, na sifa njema zote ni zake.'' ....Hupandiwa mtende peponi.

Na amesema Mtume (s.a.w): ''Ewe Abdallah bin Qais, hivi nikufahamishe (nikuonyeshe) hazina miongoni mwa hazina za pepo? Nikamwambia: Ndio Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, akaniambia, Sema: ''Hakuna uwezo wala nguvu ila za Mwenyezi Mungu,'' (ila kwa kuwezeshwa na Mwenyezi Mungu).

Na akasema Mtume (s.a.w): ''Bora ya maneno kwa Mwenyezi Mungu ni manne'': ''Ametakasika Mwenyezi Mungu, na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mkubwa.'' ....Si vibaya kuanza kwa lolote katika hayo.

Alikuja mtu mmoja wa shamba kwa Mtume (s.a.w) akamwambia, nifundishe maneno nitakayo yasema, Mtume (s.a.w) akamwambia: Sema: ''Hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila ni Mwenyezi Mungu hali ya kuwa peke yake, wala hana mshirika wake, Mwenyezi Mungu ni Mkubwa tena sana, na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu tena nyingi sana, Ametakasika Mwenyezi Mungu Mwenye Kutukuka, Mwingi wa Hekima.'' ......Yule mtu kisha akasema, Haya ni ya Mwenyezi Mungu, ni yapi yangu? Mtume (s.a.w) akamwambia, Sema: ''Ewe Mwenyezi Mungu, nisamehe, na unirehemu, na uniongoze, na uniruzuku.''

Aliku mtu akisilimu, Mtume (s.a.w) anamfundisha kuswali kisha anamuamrisha kuomba kwa matamshi haya: ''Ewe Mwenyezi Mungu, nisamehe, na unirehemu, na uniongoze, na unipe afya njema, na uniruzuku.''

Bora ya dua ni mtu kusema: (Alhamdu liLLahi). ''Kila sifa njema ni za Mwenyezi Mungu.'' Na bora ya utajo (uradi) ni mtu kusema: (Laa ilaha ila LLah). ''Hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila ni Mwenyezi Mungu.''

Mema yasioisha ni: ''Ametakasika Mwenyezi Mungu, na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila ni Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mkubwa, na hakuna uwezo wala nguvu ila za Mwenyezi Mungu, (ila kwa kuwezeshwa na Mwenyezi Mungu).''

API