Dua za kufungulia sala

Ewe Mwenyezi Mungu niweke mbali na madhambi yangu kama ulivyoweka mbali baina ya mashariki na magharibi, Ewe Mwenyezi Mungu nitakase na madhambi yangu kama vile inavyotakaswa nguo nyeupe kutokana na uchafu,Ewe Mwenyezi Mungu nisafishe na madhambi yangu kwa theluji na kwa maji na kwa barafu.

Kutakasika ni kwako Ewe Mwenyezi Mungu, na sifa njema zote ni zako, na limetukuka jina lako, na utukufu ni wako, na hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki, asiyekuwa Wewe.

Nimeuelekeza uso wangu kwa yule ambae ameumba mbingu na ardhi hali ya kumtakasia yeye dini yangu, na sikuwa mimi ni katika washirikina, hakika swala yangu na kuchinja kwangu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe vyote, hana mshirika, na kwa hilo nimeamrishwa, nami ni katika waislamu, Ewe Mwenyezi Mungu, wewe ndie mfalme, hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa wewe, wewe ndie Mola wangu na mimi ni mja wako, nimeidhulumu nafsi yangu, na nimekiri madhambi yangu kwa hivyo nisamehe madhambi yangu yote, hakika hakuna mwenye kusamehe madhambi isipokuwa wewe, na niongoze katika tabia njema (nzuri) kwani hakuna mwenye kuongoza katika tabia nzuri isipokuwa wewe, niepushe na tabia mbaya, kwani hakuna mwenye uwezo wa kuniepusha na tabia mbaya isipokuwa wewe, naitikia wito wako, na shari haitoki kwako, mimi nimepatikana kwa ajili yako, na nitarudi kwako, umetakasika na umetukuka, nakutaka msamaha na ninarejea kwako (kwa kutubia)

Ewe Mwenyezi Mungu, Mola wa Jibriil na Miikail na Israafil, Muumba wa mbingu na ardhi, Mjuzi wa mambo yaliyojificha na yaliyowazi, Wewe unahukumu baina ya waja wako katika mambo ambayo walikuwa wakitofautiana, niongoze mimi kwenye haki katika yale waliyotofautiana kwa ruhusa yako, hakika Wewe unamuongoza umtakae kwenye njia iliyonyooka.

Mwenyezi Mungu ni mkubwa, Mwenyezi Mungu ni mkubwa, Mwenyezi Mungu ni mkubwa, sifa njema ni za Mwenyezi Mungu, kwa wingi na sifa njema ni za Mwenyezi Mungu, kwa wingi, na sifa njema ni za Mwenyezi Mungu, kwa wingi, na ametakasika Mwenyezi Mungu asubuhi na jioni. (atasema maneno haya mara tatu). Najilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na shetani, na kupulizia kwake, na kutabana kwake na kutia kwake wasiwasi katika nyoyo za binadamu.

Mtume (s.a.w) alikuwa akiamka usiku ili kufanya ibada anasema: Ewe Mwenyezi Mungu ni zako sifa njema, Wewe ndie nuru ya mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake, na ni zako sifa njema wewe ndie sababu ya kusimama kwa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake, na ni zako sifa njema wewe ndiwe Mola wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake, na ni zako sifa njema, ni wako ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake, na ni zako sifa njema wewe ndiwe Mfalme wa mbingu na ardhi, na ni zako sifa njema wewe ni Haki (Kweli), na ahadi yako ni ya kweli na neno lako ni lakweli, na kukutana na wewe ni kweli, na pepo ni kweli, na moto ni kweli, na Mitume ni kweli, na Muhammad ni kweli, na Qiyama ni kweli, Ewe Mwenyezi Mungu, kwako nimejisalimisha, na kwako nimetegemea, na wewe nimekuamini, na kwako nimeregea, na kwa ajili yako nimeteta, na kwako nimehukumu, kwahivyo nisamehe niliyoyatanguliza, na niliyo yachelewesha, na niliyo yaficha, na niliyo yatangaza, Wewe ndie mwnye kuchelewesha, hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa wewe.

API